Hii ni sehemu ndogo tu ya mji wa Bukoba. |
Ujio wa vyuo vikuu katika mji wa Bukoba ambayo ni makao makuu ya mkoa wa Kagera ni moja ya mambo ambayo ninayaona kuwa ya kimaendeleo na changamoto katika mkoa huu hasa Bukoba Mjini. Kwa kipindi kirefu sasa mkoa huu umekuwa nyuma kimaendeleo japo wasemekana kuwa hazina ya wasomi na mali asili nyingi ambazo kama hivi vingetumika kiufasaha basi usingekuwa hapa ulipo sasa kimaendeleo.
Lakini hasa ninachotaka kuangalia zaidi katika suala zima la ujio wa vyuo vikuu ni suala zima la "ni nini faida na hasara za ujio wa vyuo hivi" na ni jinsi gani twaweza punguza madhara na kutafuta manufaa zaidi katika ujio huo.
Katika siku za hivi karibuni twatumainia NDAKI YA MTAKATIFU AGUSTINO TANZANIA (St. Augustine University of Tanzania) wafungue tawi lao kilipokuwa chuo cha ualimu St. Francis Nkindo nje kidogo ya mji wa Bukoba. Wakati huo huo bado maandalizi ya Ndaki ya Tumaini itakayoitwa Josiah Kibira University Collage (JOKUCo) yakiwa kwenye hatua za mwisho.
Nilipata sikia Askofu Nestory Timanywa na Msaidizi wake Askofu Methodius Kilaini wamekwenda elimisha watu Dar es Salaam kuhusu chuo kinachoanza Bukoba. nilishangaa sana, nikajiuliza watakaonufaika zaidi na chuo hiki ni watu wa dar ama wa Bukoba? je ni elimu gani wametoa kwa wana Bukoba ili kujihadhari na yatakayotokea kulingana na ufunguzi wa vyuo hivi? Ni vema sasa wananchi wakajua ni nini faida na madhara ya uwepo wa vyuo vikuu katika maeneo yao ili kuwawezesha kujua ni nini wafanye katika kijikinga dhidi madhara yake na kujipanga zaidi katika kujua wananufaika vipi na ujio wake.
Ni suala lililo wazi kuwa uwepo wa vyuo vikuu mjini Bukoba utasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza kiwango cha elimu kwa wakazi wa mji huu, kodi za mapato kwa sekta husika, Ajira na Kukua kwa uchumi wa wananchi na mji kwa ujumla.
Hata hivyo ujio wa vyuo hivi pia utakuwa na hasara zake kama kuchangia migogoro ya ardhi, biashara, ongezeko la matukio ya kihalifu, mfumuko wa bei katika bidhaa zinazopatikana humu mjini, kutokana na misuguano ya wenye pesa na madaraka kutaka kuwanyonya wale wasionacho na baadhi ya watu kujiingiza kwenye mahusiano ya kimapenzi na wanavyuo hivyo kuleta ongezeko la maambukizi ya magonjwa kama VVU/UKIMWI na magonjwa ya zinaa, mimba za utotoni, ndoa kuvunjika na ongezeko la watoto wa mitaani katika mji wa Bukoba.
Swali kubwa ambalo bado najiuliza ni Je, Halmashauri ya Manispaa ya wilaya hii hasa kwa eneo la mji huu wamejipanga kwa kiasi gani katika kukabiliana na matatizo haya na kujiimarisha katika mipago miji ili mji usizidi kutokuwa na mipango na kuwa na vichochoro vingi vya kuongeza matukio ya uhalifu na hofu ya Raia wa kawaida na wanachuo kwa ujumla?
Pengine kati ya mambo nawaza ni kuweza saidia wazazi na wanandoa kwa kuwashauri kukaa na watoto wao na kuwaeleza namna wanavyoweza kujilinda dhidi ya vishawishi vinavyotolewa na wanafunzi. Na hii ianzie kwenye ngazi ya familia ili kuwia rahisi hata watoto kuelewa.
Pia kutoa ushauri kwa Jeshi la polisi kuweka vituo vya polisi karibia na maeneo ya chuo kwa ajili ya kulinda mali za chuo, wanachuo na raia ambao wanategemea kuweka miradi itakayowanufaisha kwa ujio wa vyuo hivi itakayowawezesha kujiendeleza kiuchumi wakati huo wakivisaidia vyuo na wanachuo kujipatia mahitaji yao kwa karibu. Kwa maana hiyo basi Jeshi letu liwe makini sana katika ulinzi likisaidiana na wananchi katika kuleta maendeleo na sio kwenda kinyume na hayo kwani Jeshi hili limepewa dhamana ya kutulinda na sio kutuwinda.
Natumai kama haya yatatekelezwa na mengine mengi ambayo sikuweza yataja basi tutatarajia kuwa na maendeleo chanya yatokanayo na ujio wa vyuo katika mji wetu na kuvutia wawekezaji na wageni wengi kufika huku.
NAWATAKIENI KILA LAKHERI KATIKA KUFANIKISHA MIPANGO YOTE HII.
Ni darasa bomba kweli..ujumbe huu ilibidi usomwe na wengi. Ni kweli kabisa ulichosema.
ReplyDelete