Friday 2 December 2011

UKWELI UKO WAPI?

Labda kwa vile nimo ndani ya moja ya nchi masikini kiuchumi hivyo naweza shindwa onyesha wazi ulipo ukweli juu ya maendeleo ya nchi hizi masikini Duniani.
Tokea kuwako kwa Kambi mbili zenye nguvu na zinazokinzana Duniani kambi ya mfumo wa nchi za kibepari na Kambi ya mfumo wa nchi za Kijamaa, kumekuwako na maonevu na unyonyaji mwingi sana dhidi ya nchi zinazoendelea ufanywao na mataifa makubwa na yenye nguvu kiuchumi.



Mgawanyiko wa kambi hizi mbili ulikuwako tokea mapinduzi ya Urusi ya mwaka 1917 lakini ukaja kukua baada ya Vita vikuu vya pili vya Dunia ambapo kambi hizi mbili zilizidi pingana kiitikadi na kijeshi.

Kambi ya Kibepari iliongozwa na Marekani na kambi wa Kijamaa iliongozwa na Urusi. Katika kambi hizi, mataifa masikini yaliingizwa kwenye mikataba ya kujiunga na kambi moja wapo japo baadhi ya mataifa yalikataa kujiunga na kambi hizo na kuanzisha ushirikiano wan chi zisizofungamana na upande wowote.



Mataifa masikini, yamekuwa yakijaribu kutafuta uhuru wake wa kisiasa na kiuchumi kwa njia ya amani na utulivu, lakini yamekuwa yakiwekewa vikwazo vingi kutoka katika mataifa yale yaliyoendelea kiuchumi na kisiasa hata kufanyiwa maamuzi ambayo pengine yamediriki hata kwenda kinyume na Haki za Binadamu.



Nchi hizi (masikini) zimekuwa zikikosa msimamo wao thabiti na hata kubanwa kwa kila njia katika Nyanja za uchumi na siasa kwa kufanyiwa maamuzi. Kwa mfano kila tunachozalisha tunanauza kwa bei ya kupangiwa na ambayo ni ya chini sana katika soko la kimataifa na kila tunachonunua kikiwa ni cha bei Ghali. Kwa maana hiyo basi naweza sema kuwa Jitihada zote za nchi masikini za kutaka kujikomboa na kujitafutia maendeleo zinaonekana kuwa ni kazi bure kama hatutaweza kujitegemea na kuzidi kuzihusudu na kuzitegemea nchi tajiri zitusaidie katika kilio chetu cha kujiokomboa bila sisi wenyewe kuwa na mipango madhubuti na kuifanyia kazi.



Nchi changa hazina budi kuanzisha mikakati mbalimbali itakayowezesha kujikomboa kikamilifu. Kwa mfano uanzishwaji wa umoja wa soko nafuu wa bidhaa zetu, uimarishwaji wa njia za mawasiliano na uchukuzi, ulinzi wa pamoja hayo ni baadhi tu ya mbinu zinazoweza kusaidia katika kuleta ukombozi katika mataifa masikini.



Viongozi nao hawana budi kuungana kwa kauli na vitendo. Hakuna sababu ya kuyaogopa mataifa makubwa kiuchumi kwani kitendo hicho ndicho kinayafanya mataifa mengi Masikini kuwa vibaraka wa mataifa hayo.



Hivyo basi, Mataifa masikini kokote Duniani hatuna budi kuungana kwa hali na mali hadi tone la mwisholimekombolewa kutoka kwenye uonevu, mateso na kunyanyaswa na mataifa haya makubwa kiuchumi kwani

“MBINU ZA KUJIKOMBOA ZINAPATIKANA KWENYE UWANJA WA UKOMBOZI (MAPAMBANO)”.

Mapambano yakiendelea ushindi ni lazima.