Wednesday 22 December 2010

NIIKUMBUKAVYO MIMI DESEMBA 23, 1999.

Picha ya ajali

Ikiwa mida ya saa kumi na moja jioni, tukiwa nyumbani kijijini (NYAKIBALE) Baba aliniita na kunituma kwa Baba mkubwa katika kijiji cha jirani. Nikiwa huko mala nikapata tetesi kuwa kaka yetu mkubwa Mubelwa T, aliyekuwa safarini kutokea Dar kuja nyumbani Bukoba kapata ajali. Katika kupeleka ujumbe kwa Baba pia nikajikuta nikilieleza hili ndipo kuulizwa  kapatia wapi hiyo ajali na kusema sijasikia ni wapi kwani sikulichukulia suala la ajali kama jambo zito kutokana labda na kutokujua ajali ilikua ni nini kwa wakati huo. Nikaagizwa tena kwenda uliza hiyo ajali imetokea wapi?
Nilienda mbio bila kujali kama ni kweli ila nikihisi ni ile hali ya undugu ndio ilikua ikinisukuma kufanya yale yote na nilipofika nikaelezwa kuwa imetokea maeneo yaitwayo IGOMBE takribani kama kilometa 30 kutoka nyumbani tulipokuwa.
Ikumbukwe kwamba hiki kilikua ni kipindi cha maandalizi ya sikukuu za Krisimas na Mwaka mpya hivyo kila jambo lililohusiana na ajali hata leo huwa haliombewi ili ndugu, jamaa, wapenzi na hata wazazi wetu wasafiri na kufika na kusherehekea salama kwa pamoja huku wakifurahi, hivyo kupeleka taarifa ile ilileta hisia sana kwa wote hasa wazazi waliojua kabisa maneno yaliyosemwa na mototo kama mimi (kwa kipindi hicho) hayakua ya kujitungia.
Ilibidi Baba yetu mzazi aende kituo kidogo cha Mabasi cha pale kijijini kwetu kumsubiri mgeni akijua kuwa kwamba atakua kachukua gari jingine na muda mfupi atampokea mwanae. Kitendo cah kufika hapo stand ndogo ndipo lilikuja gari moja na hata kabla ya kuuliza kama kweli kuna ajali imetoke pale nilipomueleza, alishtushwa na habari kutoka kwa moja wa madereva aliyesikika akisema “aliwo eajali ya TAWFIQ yatokea Kenya ngu n’omwana wa Ta Bandio Mubelwa yaba alimu” (Eti kuna ajali ya gari la TAWFIQ imetokea Kenya na inasemekana hata Mubelwa motto wa Mzee Bandio alikuwemo.
Bila ya kujua nini kiliendelea Baba aliagiza mtu kuja kutueleza kuwa ajali imetokea Kenya na sio nilipoelezwa mimi na alipanda mojawapo ya magari yaliyotoka Gulioni kupeleka mizigo ya wafanya biashara na kwenda hadi mjini katiha ofisi za Tawfiq kupata habari. Kufika pale akakuta habari ni za kweli lakini jina la Mwanae halipo katika pande zote tatu yaani, wazima, majeruhi wala Waliofariki. Kuuliza namba za gari kwa wakina dada akatajiwa zile zile za gari lililopata ajali.
Kiukweli waweza pata picha ni vipi alikua akihangaika, ila kumbe jina lilikuwepo kati ya wale majeruhi sema tatizo lilikua ni jinsi gani alilitamka kutokana na kupata jeraha la ulimi.
Ilikua ni stori ambayo kiukweli ilihuzunisha sana hasa familia baada ya kupewa hizo habari lakini tulishukuru Mungu kumwona yu mzima japo alikua na majeraha yenye maumivu yaliyotokana na ajali. Nakumbuka tulipopelekwa (mimi na pacha wangu) kumwona kiukweli wote tuliishia kukumbatiana na kulia jambo lililowafanya hata wazazi kulia huku wakituachanisha. Alitueleza Mengi kuhusiana na safari hata kutupa salamu kutoka Dar es salaam. Sasa ni miaka kumi na moja tokea ajali kutokea, tuna mengi ya kumshukuru Mungu kwa kumnusuru kaka yetu kwani tumeweza jifunza mengi kupitia yeye na hasa kupitia BLOG yake ya www.changamotoyetu.blogspot.com
Kwako kaka hatuna budi kuikumbuka siku hii na twamshukuru Mungu kwa kukunusuru katika ajali hiyo. “U MEAN ALOT TO US AND WE REAL APPRECIATE YOU” sijui ni kwa jinsi gani naweza eleza umuhimu wako kwetu kama familia na hata rafiki kupitia msaada wako wa halii.akili na mali kupitia blog na hata njia nyingine kwani najua umetufunza wengi na bado naamini kuna mengi ya kujifunza kutoka kwako.
Tuikumbukapo  siku hii nipende kukuhakikishia kuwa sisi kama Familia WE ARE PROUD TO HAVE SUCH KIND OF BROTHER AND WE ARE ALL PRAYING FOR YOU.

TWAKUPENDA SANA KAKA MUBELWA NA MUNGU AKUBARIKI WEWE NA FAMILIA YAKO.


BLESSED FAMILY OF MR SIMON BANDIO.

Sunday 28 November 2010

WAPI UPINZANI WAELEKEA?


Ni majadiliano yaliyodumu kwa Takribani saa tatu kujadili Mustakabali wa vyama vya upinzani Bugeni Dodoma  ulioandaliwa na kampuni ya Vox Media na East Africa Business & Media Training Institute (EABMTI) wakitaka kujua HATMA YA UPINZANI NCHINI. Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mh. Freeman Mbowe, na aliyekuwa kiongozi wa 
nafasi hiyo katika Bunge lililopita Mh. Hamad Rashid (CUF) walichuana vikali katika mdahalo huo wa wazi uliofanyika mjini Dar- Es Salaam katika hoteli ya Movenpick na kurushwa moja kwa moja na kituo cha Televisheneni cha ITV pia kusikika kupitia RADIO ONE.

Ukiendeshwa kwa mada iliyosomeka kama "KAMBI YA UPINZANI NA TANZANIA TUNAYOITAKA," lengo kuu hasa lilikua ni kujadili mambo yaliyoibuka "mjengoni" ambapo imeonekana upinzani umeshindwa kuwa na "Kauli Moja," katika kudhihirisha mpasuko huo na kukosa kauli, tumeshuhudua mambo ya ajabu ambapo waheshimiwa hao waligeuza ukumbi huo wa wazi kuwa jukwaa la kujibizana kwa jazba hali iliyoonyesha dhahiri kuwa,hawakua wamejiandaa kwa ajili ya mdahalo huo ama upinzani bungeni ni kwa ajili ya maslahi ama binafsi au ya vyama 
wanavyotumikia na sio Taifa kama wagombea wanavyodai na wananchi wengi wanavyoamini. Binafsi nilisitisha kuangalia/sikiliza (kwa muda) pale Mh. Hamad alipomwambia Bosi wake ( Mh. Mbowe) asicheze na mwanasiasa mkongwe (yeye) jambo lililoleta vurugu na kelele kutoka kwa washiriki ambazo zilimlazimu Mwenyekiti wa Mdahalo huo Ndugu Rose Mwakitwage kusitisha kwa muda MDAHALO huo ili kutuliza vurugu hizo. 

Hakika naweza sema "ni usanii tu" ndio wafanyika katika kuunda kambi ya upinzani maana haiwezekani mafahari wawili wagombaniao madaraka kukaa na kuunda kambi iliyo makini bila ya kuwa na mwongozo mmoja wenye kueleweka. 

Yaliongelewa mengi ila zaidi ni "mpasuko wa kidini" ulioongelewa sana kipindi cha kampeni na sasa kuonekana  sio tu kuwatenganisha wananchi bali kupenyeza mizizi yake hata kwa hawa viongozi wetu huko Bungeni. Haya yalidhihirika pale Mh. Hamad alipokuwa akijibu swali la mmoja wa washiriki aliposema aliwahi ulizwa kama kambi ya upinzani itakua na nguvu ya pamoja kwani anaona  CUF imeegemea kwenye UISLAMU zaidi nae kujibu kuwa anaona CHADEMA imeegemea kwenye UKATOLIKI zaidi jambo ambalo latia mashaka kama kuna kupatana na kutimiza malengo ya upinzani pale wanapotaka kutimiza ilani zao kama chama ila kimuungano ambao naweza sema ni wa-KINAFIKI ilhali kila mmoja akimuhukumu mwenzake kidini.

Haya ni machache waliogusia viongozi hawa wakijitahidi ficha hasia zao ambazo kwa hakika walishindwa zizuia kwa ajili ya kutetea maslahi ya vyama vyao. Swali ni, Je,twajifunza nini kutoka kwa ndugu zetu hawa na mfumo mzima wa vyama vingi? Je kuna haja ya kuwepo kambi ya upinzani isiyo na kauli moja juu ya mustakabali wa nchi? Na akija mwingine na kuzungumzia mgawanyiko iwe kielimu, kikabila ama vinginevyo, tutakuwa twajenga kambi ya aina ipi katika Bunge na twawafundisha nini hawa tunaowatawala kama sio kuzidisha mpasuko? 

Kwa kuwa na lengo moja la kudai mabadiliko ya Katiba ( kama wanavyodai) ila njia tofauti za kufikia malengo mkijiita wamoja ni bora kuwaeleza kuwa MWAPOTEZA MUDA KWA KUDANGANYA WAPIGA KURA WENU mkitafuta kuimarisha maslahi na nguvu ya vyama mtokavyo.


 Angalizo kwa wananchi ni        kutoshabikia vyama kwa udini   kisa viongozi wamesema ama sivyo                       "HATUNA NCHI."


Saturday 27 November 2010

Welcome to Kato's Blog.

Ndugu Kato  Bandio in BISMARK ROCKS Mwanza.
Karibuni sana kwenye Blog hii, kutakuwa na mengi mazuri ya kujadili pamoja nanyi. Natumai yatakuwepo mengi yahusuyo jamii zaidi, na zaidi  maisha halisi ya kuigiza tunayoishi sasa na natumai kupitia kijiwe hiki tutaweza kutafuta suluhisho pamoja ama kwa kutoa mapendekezo yatakayoleta mabadiliko kwa mtu mmoja mmoja ama jamii kwa ujumla. Karibuni Kijiweni wapendwa na Mungu atusaidie wote. PamoJAH Daima